Na Mwandishi wetu ,Kigamboni
Kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani Tarehe 8 machi 2022, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Taifa Ndg. Victoria Charles Mwanziva Leo Tarehe 3 Machi 2022 ameshiriki utoaji wa Elimu kwenye Kambi maalumu ya Mabinti iliyoandaliwa na Taasisi ya Mwanamke na Uongozi ikishirikiana na Wasafi Media katika Wilaya ya Kigamboni.
Katika Mafunzo hayo yaliyobeba dhima ya Mwanamke na Uongozi "Mwanamke Makini, Nguvu ya Maamuzi", Ndg. Mwanziva ametoa mafunzo mbalimbali kwa Mabinti namna ya kutumia Fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Mazingira yanayayowazunguka na mitandao ya kijamii.
Aidha Ndg. Mwanziva amesisitiza kuwa wanawake ni nguzo kubwa na wanamapinduzi wa kweli kwenye Taifa lolote Duniani na jamii inayotuzunguka akitolea mfano uongozi imara wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameonekana kama nuru kwenye mwelekeo mpya wa maendeleo Kwa Taifa letu Kwa kusema;
"Huko Nyuma ilionekana ni vigumu sana mwanamke kushika nafasi kubwa ya uongozi jambo ambalo sio kweli, lakini leo hii kwenye Taifa letu tunaye Rais Mwanamke na Kazi yake tunaiona imetukuka kweli kweli na kila Matanzania anajivunia uwepo wake".
Pia Ndg. Mwanziva amewataka mabinti kuwa na tabia ya kujisomea vitabu mbalimbali vyenye dhima za uongozi kama njia ya kujifunza na kujiongezea maarifa kwenye mambo mahususi ya fursa na uongozi.
Vilevile Ndg. Mwanziva amewataka mabinti kutumia mitandao ya kijamii kwa makini na kuchagua aina taarifa za kuzifuatilia ili waweze kujijenga na kukua zaidi kiuongozi.
Sanjari na hilo amewaasa mabinti kutokukatishwa tamaa kwenye safari zao za mapambano ya kuleta mapinduzi ya kimaendeleo usawa katika jamii na masuala ya uongozi.
Ndg. Mwanziva ameelezea na kufundisha namna ya kuzipata fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia mitandao ya kijamii, fursa hizo ni kama, Scholarships za kusoma vyuo mbalimbali vya kimataifa, Mafunzo na mijadala mbalimbali ya uongozi na ujasiriamali, na fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia mashirika ya kimataifa na balozi mbalimbali zilizopo nchini.
Katika kuhakikisha kuwa wakati wa utafutaji wa fursa hizo kwa mabinti ku-apply ametia msisitizo kwenye ujazaji wa taarifa binafsi kwa usahihi, Ili kukidhi vigezo vya kuchaguliwa na kuzipata fursa hizo muhimu kama nafasi za kujitolea kwenye mashirika ya kimataifa, kazi, masomo, mafunzo ya mitandaoni, na ujasiriamali kama nyezo muhimu ya kukua na kujijenga kama Binti mwenye ndoto kubwa.
Mwisho Ndg Mwanziva amewapongeza sana Wasafi Media kwa kuandaa kambi hiyo maalumu kwa ajili ya kuwajenga mabinti na kuwafungulia milango mbalimbali Ili waweze kujijenga na kukua katika nyanja mbalimbali kiuchumi, kijamii na kisiasa. Lakini pia Ndg Mwanziva amewapongeza mabinti hao Kwa nafasi hii adhimu waliyoipata kukaa kambini na kujifuza na kuwasihi kutumia hii kama fursa nyingine ya kujenga mahusiano ya pamoja katika jitihada zao mbalimbali za kimaisha.
No comments:
Post a Comment