WAHADHIRI ONGEZENI MACHAPISHO YA TAFITI-PROF MKENDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 26, 2022

WAHADHIRI ONGEZENI MACHAPISHO YA TAFITI-PROF MKENDA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda akizungumza wakati akifunga mkutano wa wadau wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Sera ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu nchini leo Agosti 26,2022 Jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Maulilio Kipanyula akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Sera ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu nchini leo Agosti 26,2022 Jijini Dodoma
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Aloyce Kamamba akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Sera ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu nchini leo Agosti 26,2022 Jijini Dodoma

Na Okuly Julius Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amewataka Wahadhiri wa vyuo vikuu hapa nchini waongeze machapisho ya tafiti katika majarida makubwa duniani.

Chapisho hizo zitawawezesha kutambulika ulimwenguni kama watafiti wabobezi na kujipatia fedha hadi kiasi cha shilingi milioni hamsini.

Prof.Mkenda ameyasema hayo wakati akifunga mkutano wa wadau wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Sera ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu nchini leo Agosti 26,2022 Jijini Dodoma na kusema kuwa kwa sasa wahadhiri wengi wanaogopa sana kufanya tafiti hasa zile za kisayansi.

"Hatutaweza kwenda kwenye maeneo yote kwa wakati mmoja tunataka tuanze na utafiti wa elimu tiba,sasa hivi watu wanaogopa kufanya utafiti wa muda mrefu kutokana na ufinyu wa bajeti hivyo kwa kulitatua hilo tumetenga bilioni Moja ambapo Kila mtafiti atakayekidhi vigezo atapata Shilingi milioni 50,"amesema Mkenda

Sambamba na hayo Prof.Mkenda amesema ulimwengu wa sasa hauwezi kuepukana na masuala ya sayansi na Teknolojia hivyo kutaka wadau wote kuchochea udadisi na ubunifu kwa watoto ili baadae waweze kuajirika na kujiajiri.

"Tunataka kuvutia vijana wenye uwezo mkubwa wasome masomo ya sayansi na ili tufanikiwe katika hilo lazima tuwekeze katika elimu kwa kufuata misingi ya sayansi,ubunifu na Teknolojia,"amesisitiza Mkenda

Katika hatua nyingine Prof.Mkenda amesema kuwa wizara hiyo ipo mbioni kutambulisha mpango wa ufadhili wa masomo wa "Samia Scholarship"kwa wanafunzi bora 600 waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuona wanafunzi wengi wanakwepa kusoma masomo hayo na kuelekeza nguvu kwenye masomo mengine hali inayodidimiza masuala ya Teknolojia na ubunifu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Aloyce Kamamba ameiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuyafanyia kazi maoni ya wadau pamoja na kuzichukua,kuzitambua,kuzifadhili na kuziendeleza bunifu zinazobuniwa.

Pia amesema kuwa mawazo yaliyotolewa na wadau yasibakie katika makaratasi yafanyiwe kazi ili kutatua changamoto zilizopo katika jamii kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

" Sera hizi zisibakie tu kuwa zimeandikwa kwenye makaratasi kwani mkutano huu wa wadau utakuwa umefanyika bure kwani lengo kubwa ni kutaka kuona ni namna gani sayansi,teknolojia na ubunifu inakwenda kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii,"Amesema Kimamba

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Maulilio Kipanyula amesema kuwa wamepokea maoni kutoka kwa wadau kuhusiana na kuhuisha rasimu ya Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment