HALI YA UPATIKANAJI WA MBOLEA MKOANI MARA INARIDHISHA-TFRA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 1, 2022

HALI YA UPATIKANAJI WA MBOLEA MKOANI MARA INARIDHISHA-TFRA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo ( kushoto) akisalimiana na Afisa Kilimo Lazaro Butiliku mara baada ya Mkurugenzi kuwasili katika Ofisi za Mkoa wa Mara kufuatilia masuala mbalimbali kuhusu mbolea za ruzuku Oktoba 31, 2022
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo ( mwenye kofia) akimsikiliza Kaimu Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mara Levin Magera mara baada ya Mkurugenzi kuwasili katika Ofisi yake kufuatilia masuala mbalimbali kuhusu mbolea za ruzuku Oktoba 31, 2022
Wakala wa mbolea za ruzuku Mkoa wa Mara, Puna Agrovert (kushoto) akizungumza na msambazaji wa mbolea wa kampuni la Yara Haji baada ya kuunganishwa na Mkurugenzi wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo ili aweze kupatiwa mbolea na kuuza kwa wananchi wa Mkoa wa Mara katika mpango wa mbolea za ruzuku kwa mwaka 2022/2023 unaoendelea nchini na hivyo kuongeza mawakala wa mbolea mkoani Mara.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Ziwa, Hanafi Mohamed akieleza uwepo wa Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo (wa kwanza kushoto) mkoani humo walipofika ofisini kwa Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mara Levin Magera (hayupo pichani) Oktoba 31, 2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (Mwenye kofia) akimsikiliza Afisa Mazao wa Halmashauri ya Tarime, Sadoki Matayo ( wa pili kutoka kushoto) baada ya kufika katika jengo linalotumiwa na kampuni la ETG kuuza mbolea kwa wakulima, kama inavyoonekana mbolea ipo ya kutosha katika chumba hicho Oktoba 31, 2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (mwenye kofia ) akimsikiliza wakala wa mbolea za Ruzuku wa kampuni la Yara, Josephy Machomba ( wa kwanza kulia) alipokuwa akimpa taarifa ya biashara ya mbolea katika maeneo anayouzia mbolea wilayani Tarime mkoani Mara Oktoba 31, 2022.

Na Mwandishi wetu,Mara 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo ameridhishwa na hali ya upatikanaji wa mbolea katika Mkoa wa Mara.

Dkt. Ngailo ameonesha kuridhishwa huko baada ya kutembelea vituo vitatu vya uuzaji wa mbolea chini ya Wakala wa Mazao Mchanganyiko (CPB) vilivyopo wilaya za Rorya na Tarime na kubaini uwepo wa shehena za kutosha za mbolea za kampuni za Yara, ETG na OCP.

Pamoja na kujiridhisha na upatikanaji wa mbolea, Dkt. Ngilo amekagua maghala yaliyoainishwa na maafisa kilimo wa Mkoa wa Mara na wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya katika kijiji cha Kogaya Kata ya Ikoma yenye lengo la kuziwezesha kampuni za mbolea kutunza mbolea hizo kwa msimu wa kilimo 2022/2023 na hivyo kupanua wigo wa kufikisha mbolea kwa mkulima, kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni la mbolea na hivyo kuipunguzia mzigo serikali.

Akizungumzia kuhusu ukomo wa ekari anazotakiwa kusajiliwa mkulima, Dkt. Ngailo amesema mkulima yeyote anaruhusiwa kusajiliwa kwa heka zozote anazolima ili mradi shamba lisiwe pori aidha wakulima waliopo kwenye vyama vya ushirika (Amcos) au vilivyosajiliwa kwa umoja vinasajiliwa kwa kuweka taarifa za usajili wa vyama hivyo na ekari zinazolimwa.

Kuhusu uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima, Dkt. Ngailo amesema jitihada za wadau wote wa kilimo zinahitajika na kueleza nia ya kuyaomba makampuni ya mbolea kuwa na mashamba darasa katika maeneo mbalimbali mkoani humo ili kutoa hamasa kwa wakulima kutumia mbolea.

Akizungumza katika kikao baina ya Mkurugenzi Dkt. Ngailo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mara Levin Magera ameiomba TFRA kufanya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea katika mkoa huo kufuatia wananchi wake kuamini mbolea za viwandani zina madhara kwa udongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma I. Chikoka amesema awali wakulima hawakuwa na imani yakupata mbolea na hivyo kuwa na mwitikio mdogo wakati wa kujisajili lakini baada ya mbolea kufika wengi wamejitokeza kujisajili na wamenufaika na mbolea za ruzuku.

Chikoka amesema, kwa upande wake anaamini wakulima wa Rorya wakitumia mbolea matokeo ya mavuno yatakuwa makubwa na kusema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua Sekta ya Kilimo nchini.  

Chikoka ameshauri kuendelea kuboresha miundombinu ya usambazaji na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha jambo hili. 

“Mbolea ipatikane na usambazaji uwe rafiki nasi tunaahidi tutashirikiana kuhakikisha wakulima wapo salama” Mkuu wa Wilaya Chikoka alikazia.

Mkurugenzi Dkt. Ngailo akiambatana Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Ziwa Khanafi Mohamed amekuwa kwenye ziara ya kikazi kufuatilia upatikanaji na mwenendo wa upatikanaji wa mbolea kwa wakulima pamoja na kubaini maghala yanayoweza kutumiwa na kampuni za mbolea za Yara na Wakala wa Mazao Mchanganyiko (CPB) kusogeza mbolea karibu na wakulima katika mikoa ya Kagera, Geita na Mara.

No comments:

Post a Comment